UCHAGUZI WA AJABU
SEHEMU YA SITA
Majira ya saa mbili usiku, simu ndogo iliyokuwa mezani ilianza kuita. Aliinuka kwenye kiti na kuinyakua mezani kama mwewe na vifaranga wa kuku. Alijiuliza maswali kadhaa maana namba ile ilikuwa ngeni ila ilibidi aipokee ili ajue ilikuwa ya nani.
‘Tumefika.’ Bila hata ya salamu, ilisikika sauti kwenye simu.
‘Subiri kidogo, dakika mbili hivi.’ Alijibu Mtonyole na simu ikakatwa. Alitafakari kwa sekunde moja halafu akatafuta namba fulani kwenye simu yake.
‘Wamefika.’ Alisema kabla ya kukata simu. Baada tu ya kukata simu alifungua kabati lake na kutoa koti refu jeusi lililofika hadi kwenye magoti. Akalivaa na kisha kutoka chumbani mwake. Safari yake iliishia mbele ya gari dogo jeusi lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa bweni la wasichana. Alipolikaribia tu gari, mlango wa mbele ukafunguliwa na bila kusita akaingia ndani. Alikutana na watu wanne ambao sura zao hazikuwa ngeni machoni mwake. Hakufahamu majina ya watu wale japokuwa alishakutana nao mara kadhaa. Siku ya kwanza alipokuwa akijiandaa kupanda jukwaani kumnadi mgombea wake, alipokea simu kutoka namba ngeni. Baada ya kampeni alitakiwa kukutana na mtu fulani ambaye angeongea naye kuhusu mipango ya wapinzani wao. Alikutanishwa na kundi la watu wanne waliomuahidi donge nono ikiwa atafanikiwa kuwaletea watu kadhaa.
‘Kwanza nyinyi ni kina nani? Na mnataka watu kwa ajili ya nini? Na kwanini kazi hiyo mnipe mimi? Hapa chuoni kuna wanafunzi wengi tu, wa kike na wa kiume, kwanini mimi?’ Aliuliza maswali mengi lakini hakupewa majibu ya kuridhisha.
‘Usijali, mambo mazuri hayahitaji haraka! Utaambiwa kila kitu wakati mpango mzima utakapokamilika. Unachotakiwa kufanya ni kutafuta watu mia mbili na kuhusu mambo mengine, sisi ndiyo tutashughulikia. Kazi yako wewe ni kutafuta hao watu tu. Ukikamilisha hili jambo utapata donge nono, yaani nono zaidi ya unono wenyewe!’
‘Umeshapata wangapi mpaka sasa?’ Aliuliza mmoja wa watu wale.
‘Mia moja hamsini ila naamini kufikia kesho asubuhi tutakuwa na watu wasiopungua mia moja themanini.’ Alijibu kwa kujiamini.
‘Good!’ Alisema mwingine.
‘Kuna mpango unapikwa na kesho mtapewa utaratibu mzima wa namna ya kuutekeleza, mpango huo utatekelezwa siku ya uchaguzi, tuko pamoja?’
‘Ndiyo!’ Waliagana na Mtonyole akarudi ndani kwake.
Njiani alijiuliza maswali mengi. Hivi ni kweli hawa watu wako upande wetu? Sasa mbona siwafahamu hata majina yao? Wananiambia tu nitafute watu halafu mengine watajua wao, mhm! Wanataka watu kwa ajili ya nini? Mbona kama vile kuna kitu wananificha? Lakini hebu ngoja kwanza niwaletee hao watu halafu nipate donge langu nono na hapo ndipo mengine yatafuata.
Alipofika tu chumbani kwake, kabla hajafanya jambo lolote, alishitushwa na sauti ya mlango wa chumba chake uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. Haraka akavua koti lake na kulitupa kabatini.
‘Aaaah Muganyizi, ni wewe!’ Alisema baada ya kufungua mlango.
‘Kama unavyoniona.’
‘Mbona saa hizi na hata hukuniambia kama unakuja.’ Alisema Mtonyole kwa mashaka.
‘Tuingie ndani tafadhali.’ Alisema Muganyizi huku akisukuma mlango kuingia ndani.
‘Kuna nini?’ Aliuliza Mtonyole, akijaribu kuunganisha mawazo yake na kile kilichomleta Muganyizi usiku ule.
‘Mbona una wasiwasi sana, kulikoni?’
‘Wasiwasi! Wasiwasi wa nini?’ Alishituka na kubaki amekodoa macho kama vile alikuwa ameona mnyama mkali wa kutisha.
Alikumbuka harakati zake zote alizofanya muda mfupi uliopita. Alikumbuka tangu alipopokea simu na kuzungumza kwa muda mfupi kisha akampigia mtu mwingine na kuzungumza naye kwa muda mfupi vile vile. Alikumbuka pia jinsi alivyotoka chumbani kwake hadi kwenye gari na kurudi. Hakuona akilini mwake ni jinsi gani Muganyizi angeweza kushituka kwa kile alichokuwa amekifanya. Licha ya hayo yote, nafsi yake ilimsuta, ikamlazimisha aongee tu ukweli.
‘Tafadhali sana, naomba usimwambie kabisa Kaunda, ataumia sana!’ Alimtazama Muganyizi kisha akaendelea ‘Sina nia mbaya lakini naona nimeshikwa. Nimejaribu kukwepa mtego huu lakini nimenaswa.’
‘Kwani kuna nini?’
‘Wanataka kutumia mbinu zao zote wanazojua kuhakikisha Jamali anashinda hata kama kura zisipotosha.’
Baada ya kupita ukimya, aliendelea ‘Wanahitajika watu mia mbili ambao watatumika katika mpango wao.’
‘Kwahiyo umeshawapata?’
‘Itabidi niwatafute tu japo nimewahakikishia hadi kufikia kesho watakuwa tayari wamepatikana watu wasiopungua mia moja themanini.’
‘Nani mwingine analijua hili?’
‘Gesura.’
‘Hawakusema wanahitaji hao watu kwa ajili ya nini?’
‘Hapana, ila tu nina fikra mbaya juu ya hili.’
‘Basi sawa, huu ni mchezo kwahiyo inabidi tucheze nao. Wewe watafutie hao watu halafu mengine niachie mimi. Usijali kabisa, mimi najua namna ya kucheza huu mchezo.’
Mtonyole alibaki tu akimuangalia Muganyizi kana kwamba alikuwa anamuonya kwa hicho alichotaka kukifanya.
‘Muganyizi, naomba nihakikishie kuwa hutamwambia Makame wala Kaunda kuhusiana na hili.’
‘Kaunda ndiye Rais wa Giazi na ndiyo maana wanahangaika! Mfa maji siku zote haachi kutapatapa, nao wanatapatapa tu! Tayari wameshaona hawawezi kushinda. Wewe, Gesura, mimi pamoja na hao watu mia moja au mia mbili au mia tatu, idadi yoyote itakayokuwa imepatikana, tunatakiwa kuhakikisha Kaunda anashinda huu uchaguzi!’ Aliongea Muganyizi kwa herufi kubwa.
Hofu ilimvaa Mtonyole, alijaribu kupambana nayo lakini ilimzidi nguvu. Alijuta kujiingiza kwenye mambo ambayo yako kinyume na sheria za Chuo. Mawazo yake yote ya kupata donge nono yaliyeyuka kama barafu juani, alibakiwa na hofu tu! Itakuwaje kama Kaunda akishinda? Atabaki salama? Pindi Kaunda akigundua kuwa mkurugenzi wake wa kampeni kumbe alikuwa mpinzani wake atamuangaliaje? Aliiona hatari kubwa nyekundu mbele yake. Afanyeje? Amwambie Kaunda ukweli au anyamaze hadi atakapojua mwenyewe? Hakuwa na chaguo. Hakujua angelipata wapi.
‘Kwahiyo tufanyeje?’ Aliuliza Mtonyole.
‘Hilo, niachie mimi. Kesho asubuhi na mapema nitamtafuta Gesura niongee naye. Hao watu mia mbili watapatikana na zaidi ikibidi.’
‘Una uhakika lakini?’
‘Asilimia mia moja.’
⁂
Ndani ya chumba kimoja, Radhia alikuwa amekaa upande wa kulia, Nuru upande wa kushoto na katikati yao alikuwa amekaa Nyasuna. Hivi ndivyo ambavyo walizoea kukaa kila wakati walipokuwa wanakutana. Nyasuna alionekana ni mtu wa makamo, akiwa na miaka arobaini hadi hamsini hivi huku Nuru na Radhia wakionekana mabinti warembo, urembo ambao hata mlemavu wa macho angeweza kuuona. Wao kuwa mabinti, ilikuwa miongoni mwa sababu kubwa za kumuita Nyasuna shangazi kila mara walipomuona au kuongea naye kwenye simu.
‘Shangazi, vipi, leo hujaenda kwa mjomba?’ Aliuliza Nuru kwa utani.
‘Kwa sasa mjomba wako yuko likizo.’ Alijibu Nyasuna huku akitabasamu.
‘Shangazi!’ Radhia aliita kana kwamba ana jambo la kusema hivyo alihitaji umakini wake kwanza.
‘Niambie binti yangu.’ Alijibu Nyasuna.
‘Nategemea kuwa First Lady wa Chuo hivi karibuni.’ Alisema Radhia na wote wakaangua kicheko.
‘Jamani shangazi ! Sasa mbona unanicheka, au unaona siwezi ? Kiukweli sijapenda kabisa !’ Alideka kidogo.
‘Nyie watoto mna wazimu kweli!’ Alisema Nyasuna kisha akauliza ‘Haya na wewe unataka kuwa nani?’ Akamgeukia Nuru.
‘Mhm… Hivi mke wa Waziri Mkuu anaitwa nani vile?’ Aliuliza Nuru.
‘Mh!’ Nyasuna aliguna tu kisha ukimya ukafunika mazungumzo yao. Nyasuna akavunja ukimya, akamuuliza Nuru ‘Huwa unawasaidia wenzako kufanya kampeni?’
‘Kusema kweli…’ Alijibu huku akiweka mkono wake begani kwa Nyasuna. Alimtazama machoni kisha akaendelea ‘Mimi na siasa ni kama paka na panya. Sijui chochote kuhusiana na siasa yaani hata ninaposikia watu wanasema siasa, huwa sielewi wanamaanisha nini.’
‘Siasa ni mchezo wa hatari, tena usioaminika, unaochezwa na watu wanaotaka madaraka kwa watu wengine. Huwachezea mchezo huu kwa sera ambapo wengine hutumia hadi ujanja kwa ajili ya kuhakikisha tu wanashinda mchezo huu. Kuna mengi sana katika siasa lakini nadhani haya machache yanaweza kukupa mwanga kidogo kuhusiana na siasa.’ Alijibu Nyasuna na ukimya ukafuata.
‘Nimesikia eti Kaunda anafikiria kuachana na jambo hili.’ Radhia alivunja ukimya. Nyasuna akashituka nusura kuanguka, alibaki amekodoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango. Alimshika Radhia begani na kisha kumtazama usoni kwa huzuni.
‘Ndivyo ulivyosema ? Au ni masikio yangu ndiyo yameanza kupata matatizo, hayasikii tena vizuri ? Umesemaje ? Kaunda anataka kuachana na jambo hili ? Kwanini aachane na jambo hili?’ Maswali mfululizo yalimtoka Nyasuna.
‘Anadai Jamali anapata msaada mkubwa sana hapa chuoni, kwahiyo, anaona kabisa kuna hila zinafanyika ili ashinde.’ Alijibu Radhia akiwa ameinamisha uso wake. Alikosa furaha kabisa. Uso wake wa tabasamu hakuwa nao tena.
‘Haiwezekani ! Haiwezekani ! Haiwezekani ! Hiyo siyo sababu ya kumfanya atake kuachana na jambo hili. Anasema Jamali anapata msaada mkubwa hapa chuoni na kwamba anaungwa sana mkono, kwani yeye amejuaje kama haungwi mkono ? Nani amemwambia yeye hapati msaada ? Mbona anawahi kujikatia tamaa mapema hivyo ? Hadi leo hii bado kuna muda anaweza kufanya kampeni, sasa kwanini asifanye kampeni ?’ Nyasuna alichanganyikiwa kabisa. Alizungumza kwa masikitiko huku akiuliza maswali mengi magumu ambayo Radhia hakuwa na majibu yake. Moyoni mwake alikuwa tayari amemchagua Kaunda kuwa Rais wake. Tangu mwaka jana aliposhindwa kwa mara ya kwanza, alifanya uchunguzi wake na kwa kutumia busara zake kama mtu mzima aligundua kabisa kulikuwa na hila zilizokuwa zimefanyika mpaka Kalinga akashinda. Hapo ndipo aliamua kuwa upande wa Kaunda kwa sababu alimuona alikuwa muadilifu. Mara kadhaa alimfanyia kampeni hususani alipokutana na watu wazima wenzake. Aliwaeleza ni kwa namna gani Kaunda alikuwa anafaa kabisa kuwa kiongozi wa Giazi kwa sababu hata hivyo tangu Kalinga amekuwa kiongozi hakuna chochote kikubwa kilichokuwa kimefanyika zaidi ya mambo ya kawaida tu ambayo yangeweza kufanywa hata na wabunge. Maneno ya Radhia yalikuwa ni msumari wa moto uliopigiliwa kwenye kifua chake, ulimchoma hadi moyoni. Hakuweza kustahimili maumivu yake. Siku zote alitamani Giazi ipate kiongozi kama yule kutokana na uadilifu wake. Alipenda sana namna alivyokuwa akijieleza na umakini aliokuwa nao katika kila hoja aliyoitoa. Alitoa hoja zake na aliweza kuzitetea vizuri kabisa. Kila mara alipopinga hoja au wazo la mtu basi alipinga kwa hoja kwani siku zote alizoea kusema kuwa hoja haipigwi rungu bali inapigwa na hoja nyingine. Leo anataka kuachana na mambo ya uchaguzi eti kisa hana msaada wa Chuo? Ni msaada gani huo ambao anauhitaji? Hakupata majibu ya maswali yake.
‘Mpigie simu mwambie nahitaji kuonana naye.’ Alisema Nyasuna.
Radhia akachukua simu na kupiga na baada ya dakika kadhaa…
‘Shangazi, huyu hapa, anataka kuongea na wewe.’

Comments
Post a Comment