UCHAGUZI WA AJABU
UCHAGUZI WA AJABU
Kaunda, M
Majira hayakufanya hiyana, yalitekeleza majukumu yake yakaisha na hatimaye ilikuwa ni asubuhi tulivu ya siku nyingine iliyokaribishwa na sauti nyororo za ndege waliokuwa wakiimba kwa utukufu wa siku hiyo, walimshukuru Mungu wao kuwajaalia kuiona siku nyingine. Kwa mbali alionekana mshindi wa siku hiyo akiwa na makombe kedekede. Baada ya kupambana kwa muda mrefu, weupe wa mchana uliufunika weusi wa usiku. Ushindi huu ulikuwa na maana kubwa sana kwake kwani ulimfanya awasaidie watu kuendesha shughuli zao kwa ufanisi wa hali ya juu zaidi. Giza nalo, baada ya vita vikali, lilishindwa mapambano. Halikuwa na budi ila tu kukusanya virago vyake na kuondoka mahali pale ili kuliruhusu jua lishike nafasi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kila mchana. Popo nao hawakuzubaa, waliondoka mmoja mmoja kwenda kazini kwa sababu muda wao wa kuwa pale ulikuwa umefika ukingoni. Kwa shingo upande, walikusanya kila kilichowahusu ili kuondoka eneo lile. Walilazimika kuondoka kwa ajili ya kufanya kazi kwa ajili ya familia zao na pia kupumzika ili wapate nguvu za kurudi tena baadaye, wakati jua litakapozama. Waliondoka ili kutoa nafasi kwa wanyama na viumbe wengine nao wafurahie hewa safi pamoja na mengi mazuri yaliyopo katika ulimwengu huu wa bure na wa kipekee ambao hata hawaulipii ushuru kuishi ndani yake. Majogoo mbalimbali wa maeneo ya jirani wangewezaje kukaa kimya? Wangeachaje kuwaashiria watu kuwa masaa yameenda na sasa ni siku nyingine? Kutokuwa alama pekee ya kuashiria mwanzo wa siku mpya, bado waliamua kujiweka mbali na lawama za watu ambazo zingejitokeza dhidi yao hapo baadaye kama wangeamka kwa kuchelewa, tofauti na muda wao wa kawaida wa kuamka. Kooo! Koo! Kookooriikoo! Kookoo! Kokoriikoo! Bila kinyongo na kwa upendo wa dhati, waliashiria kuwa kulikuwa kumekucha na makucha yake!
Ilikuwa ni asubuhi shwari kabisa tena iliyotulia kama maiti mochwari huku upepo nao ukipuliza kwa kasi ya chini. Wa kuamka waliamka na wa kuendelea kuvuta shuka waliendeleza dharau zao kwa majogoo wale. Ilikuwa ni asubuhi ya siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na kwa muda mrefu na kila aliye chini ya jua lililokuwa likiangaza mahali pale kila mchana. Watu waliisubiri siku hii kwa hamu kubwa kama vile walikuwa na safari kubwa na muhimu waliyokuwa wameipanga, walitegemea kwenda Dubai au Paris au London. Miongoni mwa sehemu hizi, hakuna yoyote ambayo ilitarajiwa kufikiwa na watu hawa siku ya leo. Siku hii ilikuwa ni siku adhimu kwao kwani katika siku hii angejulikana nani ni nani katika serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Giazi.
Kadri muda ulivyoyoyoma ndivyo maandalizi kwa ajili ya siku hii yalizidi kupamba moto; wagombea, Tume ya Uchaguzi, wapiga kura na mfumo mzima wa utawala kwa ujumla. Chuo kizima kilienea mapambo kila mahali. Wanafunzi wote waliokuwa wakipita huku na kule, walipita kwenye mapambo. Wafanya usafi walifanya usafi kwenye mapambo. Walinzi hawakuwa na kazi ya kufanya zaidi ya kulinda tu mapambo. Sisimizi na wadudu wengine walifanya sherehe kubwa siku hiyo. Walikuwa wamepata mapambo ya bure. Sambamba na mapambo, kulikuwa na mahema yaliyozunguka eneo lile. GIAZI GIAZI GIAZI. Maandishi makubwa yalizunguka mahema yale. Mahema yalikuwa mengi, hayakuweza kuhesabika kama punje za sukari kwenye mchele. Giazi yote ilifunikwa na mapambo mbalimbali yaliyotosha kutoa ushahidi wa dhati kwa yeyote aliyeyaona kuwa mahali pale palitarajiwa kuwa na harusi kubwa, tena ya kihistoria.
Serikali ya Chuo haikuwa nyuma kama mkia wa mbuzi. Ilitoa agizo la kudumisha amani kuanzia mwanzo hadi mwisho wa tukio lile. Giazi yote ilizungukwa na askari wengi waliokuwa na silaha mikononi na nyingine mifukoni. Baadhi ya wapiga kura walihisi kuendesha huku wengine wakizimia kabisa, na wengine wakiingiwa na hofu na wasiwasi mkubwa kana kwamba walikuwa wamejisaidia ugenini halafu kukacha. Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Chuo cha Giazi aliligundua hilo akawatoa wasiwasi kwa kuwahakikishia kuwa usalama upo na utazidi kuwepo wakati wote. Kilichokuwa kinasubiriwa pale ni maamuzi tu ya wapiga kura. Askari wale wako pale kwa ajili ya kudumisha amani tu katika tukio hilo.
Baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika, watu walielekea ukumbini ambako ndiko wangepata matokeo. Ukumbi haukukalika, watu walisubiri kwa hamu ufike wakati wa kutangazwa matokeo. Ulipofika wakati wa kutangazwa matokeo ya urais, kila mtu alikuwa kimya akisubiri kufurahi au kuhuzunika na yule aliyekuwa amemchagua baada ya kuona anafaa kulingana na sera zake. Ni wakati huu ambapo hata Jamali, ambaye awali, alikuwa na uhakika wa kushinda kwa asilimia mia nane, tumbo lilimuuma kwa hofu na woga na alihisi kuharisha. Alitulia tu lakini roho ilimvimba mithili ya mbuzi aliyegongwa na treni. Akishinda ni wazi atafurahi sana, tena anaweza kuchinja hata ng’ombe au mbuzi kama siyo ngamia, lakini vipi akishindwa? Atachinja nini? Ataweza kuchinja bata au kuku? Ataweza kustahimili misukosuko yote itakayompata? Atakuwa na uwezo wa kuwatazama tena watu aliowahakikishia hapo kabla kuwa atashinda? Wapi ataificha sura yake? Asiposhinda uchaguzi huu maana yake juhudi zake zote zitakuwa ni kazi bure. Maswali mengi yalijengeka kichwani mwake, ambayo yote hakuyapatia majibu sahihi. Alitulia huku kijasho chembamba cha woga kikitengeneza michirizi katika tumbo lake.
Kaunda, alikuwa na huzuni sana na majonzi makubwa hata kabla ya hatua hii. Mwili wake wote ulishikwa na ganzi nzito mithili ya mtu aliyeondokewa na wapendwa wake wote, tena kwa wakati mmoja. Kichwa chake kilikuwa kizito kama gunia la kilo mia moja kwa maswali aliyokuwa ameyabeba ndani yake. Ni kwa namna gani atawakabili wanafunzi wenzake? Kila mara walizoea kumuita Profesa kutokana na muonekano wake na namna alivyomkuwa mkali katika kozi yake, sasa bado watakuwa na imani naye kama Profesa? Au sasa watamuona tu kama galasa? Ina maana hata baada ya kusoma Sayansi ya Siasa kwa mwaka mzima, maarifa hayo hayajamsaidia kushinda uchaguzi huu? Yalikuwa maswali mengi ambayo hata yeye mwenyewe hakujua wapi angepata majibu yake. Baada ya kukosa majibu yake, alikaa akajikunyata kama mbuzi aliyenyeshewa na mvua.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi alisimama akakohoa kidogo kuweka koo lake sawa kisha akazungumza machache kuhusiana na uchaguzi ule, akatoa maelekezo nini kifanyike kwa yule atakayekuwa ameshinda, na yule atakayekuwa ameshindwa, basi anatakiwa ajue kushindwa pale siyo kushindwa maisha na hata hivyo kuna maisha baada ya uchaguzi na maisha baada ya chuo. Kikubwa tu asiwe na mawazo sana, asome kwa bidii ili aweze kufaulu mitihani yake. Baada ya maneno machache, alitangaza matokeo yaliyobadilisha hali ya hewa na muonekano mzima wa ukumbi ule.
Comments
Post a Comment