UCHAGUZI WA AJABU
SEHEMU YA TATU
‘Bro, kwanini tusiachane tu na haya mambo?’ Aliuliza kwa huzuni Masenyi Kaunda baada ya ukimya mfupi tangu aingie chumbani kwa Abdul Makame. Makame alimtazama rafiki yake kwa sekunde kadhaa.
‘What’s wrong my friend?’
‘Huu uchaguzi siuelewi kabisa!’
‘Y’
‘Naona huu uchaguzi ni wa upande mmoja tu, hauhitaji upinzani. Hatuungwi mkono na uongozi wa Chuo. Ni zaidi ya mara elfu moja nimepata taarifa za Jamali kuitwa na Makamu Mkuu wa Chuo, bila shaka ameandaliwa tayari kuwa kiongozi wa chuo hiki, tutafanyaje?’
‘Kaunda, usijali rafiki yangu, nchi yetu ni ya kidemokrasia ndiyo maana tuko vyama tofauti lakini tunagombea pamoja. Uchaguzi wa chuoni una utofauti mkubwa sana na uchaguzi wa nchi, hakuna siasa zozote!’
‘Eti umesemaje? Ndivyo hivyo ulivyosema? Au mimi ndiye nimekusikia vibaya? Naona aliyekudanganya hakuna siasa kwenye chaguzi za vyuoni ameshakufa kwahiyo hakuna tena wa kukutibu. Siasa zipo sema tu wewe ndiye bado uko nyuma, you have got much to learn! Now kuna mbinu zinafanyika kupata idadi kubwa ya wapiga kura tena inaonekana hata wengine siyo wanafunzi.’
‘Haya yote umeyajuaje?’
‘Makame, siku zote mtu atakunyima chakula lakini siyo maneno! Ndiyo maana nakwambia wewe bado uko nyuma. Yaani unagombea lakini unashindwa kuwa na taarifa nyeti kama hizi? Unanishangaza sana!’
Wote wawili walikaa kimya. Kila mtu alikuwa na mawazo tofauti kichwani mwake. Kaunda alianza kuuona ugumu unaopatikana kwa yeye kuwa rais wakati Makame akiwa haamini yale aliyoyasikia kutoka kwa rafiki yake, aliona kama ni wasiwasi wake tu. Baada ya kutafakari kwa kina, Makame alimuondoa wasiwasi rafiki yake.
‘Lakini usisahau kuwa hayo ni maneno ya kuambiwa tu, na siku zote maneno ya kuambiwa yanaweza kuwa ya kweli au la!’
‘Nawe pia usisahau kuwa lisemwalo lipo na kama halipo basi linakuja. Hili siyo kwamba linakuja bali tayari limeshafika.’
Kaunda alishindwa kukaa kwenye kiti chake, aliona kiti chote kimewekwa misumari ya moto. Alianza kuzunguka chumba kizima kama popo. Kichwani mwake alikuwa na maswali mengi ambayo hakujua nani angeweza kumpa majibu. Alikuwa na wasiwasi ambao hakujua nani angeuondoa. Alikuwa na woga ambao hakujua nani angeumaliza. Alikuwa na mashaka ambayo hakujua nani angemgawia. Alikuwa na majonzi ambayo hakujua nani angemfariji.
‘Usijali ndugu, tuko vyama tofauti ila tambua umoja wetu una maana kubwa sana. Ni jambo la ajabu lisilotegemewa na yeyote, wao wenyewe wanaona kabisa tutawashinda kwa umoja huu ndiyo maana wanafanya hila zote kuhakikisha tunaanguka. Kwani umesahau kuwa umoja ni nguvu utengano ni udhaifu? Jambo moja tu la kuzingatia, wapiga kura ndiyo watatoa uamuzi.’
Hakuwa na chochote cha kusema. Aliona kama vile alikuwa anampaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Wapiga kura ndiyo watatoa uamuzi, ni kauli ambayo aliielewa lakini hakuielewa. Watatoaje uamuzi na wakati kuna mipango iko jikoni inapikwa? Watatoaje uamuzi na wakati Makamu Mkuu wa Chuo kuna kitu kwake hakiko sawa? Watatoaje uamuzi na wakati kuna watu kadhaa wameandaliwa kuongeza idadi ya kura kwa Jamali? Watatoaje uamuzi na wakati Jamali anafanya kila mbinu ashinde? Watatoaje uamuzi…… Watatoaje uamuzi…… Watatoaje uamuzi…… Hakumuelewa rafiki yake. Aliamua tu kuondoka bila hata ya kumuaga.
Njia yote aliyopita ilikuwa ndefu, angeweza kuifungia hata kuni lakini hakutaka kufanya hivyo. Wasiwasi, mashaka na kukata tamaa vilimtawala, havikutaka kutoa majeshi yake kichwani mwake. Hakuona dalili zozote za yeye kushinda. Alikumbuka vizuri changamoto zilizompiga vikumbo wakati wa kupitishwa jina lake kama mgombea.
Mikidadi na Kaunda, majina mawili pekee, yaliwekwa mezani. Baada ya kura za wajumbe, licha ya umaarufu aliokuwa nao, aliangukia pua. Uchaguzi haukuwa wa haki. Alilijua hilo. Aliamua kujikabidhisha kwa Mungu na kukiri haikupangwa aongoze chuo kile. Nafsi nyingine ilimsisitiza kukata rufaa ili yapatikane matokeo ya haki. Ilimtaka kutokata tamaa. Katika ukoo wao ilikuwa ni bora kunywa maji kukata kiu kuliko kukata tamaa. Nafsi nyingine ilimsaliti, haikumruhusu kabisa kuwa na mawazo hayo isipokuwa kumuonyesha tu hawezi kuwa kiongozi. Zote zilikuwa nafsi zake, hakujua aifuate ipi.
Aso mtu ana Mungu. Matokeo yalipokelewa tofauti na wanafunzi. Yaani Kaunda hajashinda? Kaunda huyu huyu ninayemjua mimi au mwingine? Lazima tu wajumbe wamefanya yao. Bila shaka Mikidadi ametoa rushwa ili jina lake lipitishwe. Nani asiyemjua Mikidadi? Akitaka lake lazima litimie kwa gharama yoyote. Ni mara ngapi amekaa na wajumbe vikao visivyoeleweka? Ni mara ngapi amewatoa kupata chakula cha jioni pamoja naye? Maneno mengi yalienea kwenye vinywa vya wanafunzi baada ya kupita kwenye ubao wa matangazo na kuona matokeo. Mgogoro ulizaliwa na kukua kwa kasi katika ardhi yote ya Giazi. Siku mbili pekee zilitosha kufuta amani ya Giazi iliyotengenezwa kwa muda mrefu. TUNAMTAKA KAUNDA, TUNAITAKA HAKI. KAUNDA NDIYE RAIS. KATAA RUSHWA TETEA HAKI. Wakiwa na mabango mbalimbali, walienda moja kwa moja hadi ofisi ya chama alichokuwepo Kaunda.
‘Hawa wapuuzi tu!’ Aliongea mwanafunzi mmoja kwa hasira baada ya kuona hawawezi kupata wanachokihitaji. Aliongoza msafara moja kwa moja hadi ofisi ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi. Jambo ni moja tu, uchaguzi huru na wa haki. Kuondoa vurugu chuoni, alikubali.
Chini ya usimamizi mkali wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, uchaguzi ulirudiwa. Kama walivyotarajia wanafunzi, ndivyo ilivyokuwa. Wajumbe walikiri kupokea chochote kitu kutoka kwa Mikidadi. Mikidadi na wao wote, habari zao zikasahaulika katika ardhi ya Giazi na maeneo ya jirani.
Milima, mabonde na tambarare alivuka hadi kupata nafasi ya kugombea. Kichwani mwake bado alijiuliza ni kwa namna gani ataweza kumshinda Jamali. Tayari alikuwa ameshapata taarifa kibao kuhusiana na figisu zinazofanywa ili January Jamali ashinde. Wanafunzi wengi walimpenda kutokana na roho yake ya kusaidia watu, hilo alilijua lakini bado halikumpa amani kabisa. Wasiwasi ndiyo akili, tayari alishaona kuna mipango mikubwa iliyokuwa imesukwa ili apigwe chini.
⁂
Masenyi Kaunda, kijana mrefu, mwembamba, mweusi kutoka nyanda za juu kaskazini, aliingia Chuoni miaka miwili iliyopita kusomea Sayansi ya Siasa kwa sababu alipenda sana siasa. Miwani ambayo huivaa kila mara ilimpelekea kupewa jina jingine, Profesa. Kusoma kwake Sayansi ya Siasa hakukuwa bahati mbaya. Alipenda sana siasa kutoka moyoni. Kila mara alipojikwaa au kujikata, alivuja damu iliyokuwa na siasa ndani yake. Mipango yake aliiendesha kisiasa, maneno yake yalifunikwa na siasa. Nguo zake alizivaa kisiasa. Alitembea kisiasa, alikula kisiasa, alioga kisiasa. Baba yake na mama yake walikuwa ni siasa. Mwenendo mzima wa maisha yake ulikuwa ni siasa. Vijiwe vya chini ya miti vilitoa ushuhuda namna gani aliizungumzia siasa. Alikuwa na maarifa ya kutosha kuhusiana na siasa. Alifanya vizuri sana katika kozi yake na alijiona kwenye kiti cha urais baada ya kumaliza masomo yake. Ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu. Maarifa ya kutosha kuhusiana na siasa hayakumnyima wasiwasi wa kushinda uchaguzi. Aliona tayari ameshaangukia pua.
Mwaka uliopita, aliingia katika kinyang’anyiro na Josia Kalinga lakini Mungu hakuwa upande wake kama alivyodhani ingekuwa. Ulikuwa ni ushindi uliotiliwa mashaka sana. Zilionekana dalili za udanganyifu hadi kupatikana mshindi. Japokuwa alikosa nafasi, bado aliendelea kuwa mwanachama mwaminifu kwenye chama chake. Alifanya kila awezalo kusaidia chama kwa njia mbalimbali. Daima alihakikisha chama chake kinasonga mbele. Hakukata tamaa kwani aliamini kuwa muda wake utafika na siku moja atatimiza ndoto zake. Wakati wa Mungu ndiyo wakati sahihi, alizoea kusema.
Alizishinda changamoto kadhaa na kupata nafasi ya kugombea urais. Alikutana na Abdul Makame, aliyewahi kutaka kugombea urais, ushauri wa marafiki ukamponza. Walikubaliana kuungana, Kaunda awe mgombea urais na Makame mgombea mwenza. Watu, mizimu, wanyama, majini na wadudu waliokuwepo siku hiyo walishangazwa na muungano wao. Mgombea urais na mgombea mwenza vyama viwili tofauti? Wanaaminiana kwa kiasi gani? Siasa gani ina kuaminiana kama huku? Kila sehemu kulisikika maswali ya kila aina. Huenda wanatania!
Si Kaunda wala Makame aliyewahi kurithi kwa wazazi tatizo la uziwi, walisikia vyema ila waliweka pamba masikioni wasisikie chochote. Siasa siyo uadui, walizoea kusema.

Comments
Post a Comment