UCHAGUZI WA AJABU

 

SEHEMU YA NNE

Eneo lilipambwa vizuri kumshawishi yeyote kusogea karibu kujua kulikuwa na nini. Baadhi ya watu walikuwa wamekaa katika viti vyao kwa umakini kabisa wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea mbele yao katika jukwaa dogo la ngazi tatu lililopambwa kwa vitambaa vyeupe vyenye nembo ya Giazi.

‘Ndugu zangu, tayari nimeshaongea mengi, sitaki niendelee kuwachosha zaidi. Naomba nimkaribishe mheshimiwa rais aseme nanyi.’ Aliongea Christopher na kukabidhi maiki.

‘Leeleeeleee! Leeeeleeleee! Leeeeleeeeleeeee!’ Sauti za vigelegele zilipigwa na wasichana. Walikuwa na nyuso za furaha wakimshangilia rais wao. Walikuwa wako tayari kumsikiliza kwa ajili ya maendeleo ya chuo chao.

‘Kooh! Koooh!’ Alipanda jukwaani akakohoa kidogo kuweka sawa koo lake. ‘Jamali oyeeee! Jamali safiii! Uchaguzi oyeee! Uchaguzi saaafiii! Giazi oyeeee! Giazi saaafiiii!’

‘Oyeeee! Saafiii! Leeleelee! Looloo’ Sauti za wasichana zilifunika za wavulana. Kila mara Jamali alisema sauti hazitoshi. Hawakuweza kumbishia rais wao, waliongeza sauti zao hadi wakakauka makoo na wengine walitoa sauti kwa kukoroma. Akisaidiana na Amimu Hamisi, Christopher alichukua chupa za maji akaanza kuzigawa kwa kila mmoja aliyekuwa pale. ‘Baada ya kulainisha makoo, nitawaletea soda na biskuti, huyu ndiye rais wetu, haiwezekani tumsikilize halafu tutoke kapa! Sisi siyo kama hao wengine.’

‘Kwanza kabisa, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuweka hai hadi sasa. Siyo uwezo wala nguvu zetu bali rehema zake. Kuna wengi walitamani kufikia siku hii ya leo lakini Mungu hajawapa nafasi hiyo. Kuna wengine walitamani kuifikia siku hii, kweli Mungu amewajaalia wameifikia lakini wako vitandani wamelazwa, wengine hawajitambui. Sisi kuwa hapa inabidi tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa dhati kwani ametuchagua miongoni mwa viumbe wake. Baada ya shukrani, nitaeleza ilani ya chama chetu kuwajulisha mambo ambayo yatafanywa na rais wenu…’

‘Umepitaa! Umepitaa tayari! Ooyo! Oooyoo! Leelelee! Wewe ndiye rais sasa! Hakuna tena mwingine! Mwingine fotokopi! Hatuitaki ile fimbo! Haina chake mjiniiiiii! Sauti za kila aina zilisikika. Alivuta pumzi furaha ipungue.

‘Kwanza nitahakikisha sote tunajifunza kwa ufanisi mkubwa. Baadhi ya kumbi za mihadhara zina feni tu na wala siyo viyoyozi. Feni daima haziondoi joto, tutawezaje kusoma na joto kali hivi? Hilo liko ndani ya uwezo wangu, mamlaka yangu yananiruhusu kushughulika na jambo kama hilo. Kama maktaba kuna viyoyozi basi linalowezekana maktaba hata huku kwenye kumbi za mihadhara linawezekana. Pili, nitashughulikia changamoto za fedha za kujikimu; wanafunzi wengi huchelewa kupata fedha zao hasa wale waliorudia mitihani. Kama kiongozi, ni jukumu langu kuhakikisha taarifa zao zinatumwa mapema ili wapate pesa pamoja na wenzao. Wakipata pesa pamoja na wenzao, wataweza kuepukana na vishawishi, hawatakuwa tena na haja ya kuchukua mikopo yenye riba, mikopo ambayo haiwasaidii ila kuwaumiza tu. Mara zote huchelewa kupata fedha kwa sababu ya ufuatiliaji mbovu. Nitarekebisha yote hayo.’ Aliongea mengi akaeleweka. Alitamani aendelee lakini muda ulimuangalia kwa jicho la hasira. Aliaga na kuahidi kukutana tena siku nyingine ili awajulishe alichodhamiria kufanya kuboresha maisha yao.

Usiku wa ahadi hauchelewi kukucha. Ilikuwa ni siku nyingine tulivu kabisa! Baada ya kujiandaa alitakiwa kuendelea na kampeni. Alikutana na wananchi wake wakiwa na nyuso za furaha. Alitamani kuzungumza nao mambo mazuri aliyowapendelea. Watu walikanyagana ndani ya ukumbi uliowapokea kwa bashasha baada ya hali ya hewa kuwakataa huko uwanjani. Aliwaahidi akawaahidi akawaahidi mambo ambayo angefanya baada ya kuwa kiongozi. Katikati ya kampeni, ghafla bin vu, aliona jambo la ajabu lililomuacha na maswali mengi. Mawe yalimkimbilia kwa hasira. ‘Rais wetu!’ Amimu na Christopher walipokelewa vizuri na mawe yale. Taharuki ilienea ukumbi mzima. Madirisha yaliisaidia milango kazi.

Walipofika ndani kwao hawakuwa na haja ya kuoga, walikuwa tayari wameoga maji mekundu uso mzima. Atakuwa ni nani huyu? Hataki nimalize kampeni? Hataki nishinde? Lazima tu ni adui yangu anataka kunipokonya ushindi. Dah! Ama kweli binadamu wabaya, majini wanatumwa!

‘Kweli bana, ubinadamu kazi japokuwa hatulipwi mshahara !’ Christopher aligongelea msumari.

Kama moto msituni, taarifa zilienea kwa kasi kwenye makundi mbalimbali ya WhatsApp na Instagram. Giazi yote ilitapakaa taarifa ambazo haukujulikana ukweli wake.

‘Umeshapata hizi habari?’ Lilikuwa swali la kwanza la Kaunda kwa Makame.

‘Habari gani?’

‘Ndiyo maana kila siku huwa nakwambia uko nyuma nyuma kama mkia wa mbuzi, hujui mpinzani wetu alioshwa na mawe wakati wa kampeni, watu wote waliokuwa pale walipata mawe ya kutosha kujengea nyumba.’

‘Acha utani! Acha utani ! Acha kabisa ! Nani anaweza kufanya hivyo? Mbona Giazi haina mambo ya hivi? Kila siku kampeni zinafanyika kwa amani tu.’

‘Sasa unadhani nina majibu ya hayo maswali yako? Inasemekana Gayo ndiye aliyeanzisha vurugu.’

‘Gayo?!? Gayo si mtu wetu?!? Kama ni Gayo maana yake hata sisi tunahusika kwa namna moja au nyingine kwa sababu Gayo tupo naye. Kaunda, hili jambo ni kubwa, inabidi tuwe makini sana vinginevyo tutaingia kwenye kesi bila kujua. Gayo tupo naye na sisi ndiyo wagombea, hili ni tatizo. Inabidi tuchunguze kama kweli Gayo ni mtu wetu au anajifanya tu. Hatuna uadui na Jamali, sasa kwanini tumfanyie fujo? Asiyekubali kushindwa si mshindani. Binafsi, sijui Gayo alitumwa na nani, au wewe ulimtuma?’

Hakuweza kujibu swali lile, aliinuka na kuondoka. Labda siyo Gayo, ni watu tu wenye hila wanataka kumchafua. Maneno ya Makame yalifumbua macho yake. Mwanzo hakufikiria chochote ila kwa sasa aliona hatari iliyoko mbele yake. Wao ndiyo wapinzani, kusema hawahusiki ni sawa na kumwaga sukari baharini ili maji yawe matamu. ‘Kuna haja ya kufanya utafiti wa kina kujua Gayo alitumwa na nani.’ Kichwa kilianza kuwa kizito kwa mawazo, alishindwa kukibeba. Hakuweza kumwambia Makame kilichompeleka kwake, aliondoka bila hata kuaga, tena akiwa na jambo jipya.

 

Comments

Popular posts from this blog

J’AIME LE FRANÇAIS. LIVRE DE L’ÉLÈVE POUR LA PREMIÈRE ANNÉE. ENSEIGNEMENT SECONDAIRE

UCHAGUZI WA AJABU