UCHAGUZI WA AJABU

 

SEHEMU YA TANO

Hayawi hayawi hatimaye yamekuwa! Leo ndiyo leo, asemaye kesho muongo! Leo ndiyo zitajulikana mbivu na mbichi. Maandalizi yote yalishafanyika. Ukumbi mzima ulipambwa kwa mapambo yenye rangi mbalimbali, kijani, njano, nyeusi, nyeupe, rangi hazikuhesabika. Mbele kuliwekwa mapambo yenye nembo ya Chuo kuonyesha ukubwa wa kile kilichokuwa kinaendelea. Ukumbi mzima ulijengwa kwa mapambo, ulipendeza sana kwa sababu ulikuwa kilele cha tukio zima. Nje ya ukumbi kulikuwa na uwanja mkubwa wenye majani yaliyovutia kwa rangi yake ya kijani iliyokoza kama majani ya miti wakati wa masika. Watu wasingesimama kama milingoti, viti vingi vilipangwa kurahisisha utokeaji wa tukio zima, vilifunikwa kwa mahema. Mbele ya viti baada ya uwazi mdogo, zilionekana meza zilizokuwa zimepambwa kwa vitambaa vyeupe juu yake. Juu ya vitambaa kulikuwa na masanduku kadhaa yenye picha juu yake. Masanduku yalitengenezwa yakaachiwa uwazi sehemu ya juu, uwazi uliotosha kupitisha noti ya elfu kumi. Mahema yote yalizungukwa na tepe za maneno UCHAGUZI WA HAKI, CHAGUA KIONGOZI BORA KWA MAENDELEO YAKO NA YA CHUO CHAKO. Maneno ya kuwahamasisha wanafunzi kufanya maamuzi sahihi juu ya nani wanayemchagua kulingana na namna walivyosikia sera zake.

Kufikia saa tatu na nusu, wanafunzi wote walikuwa wamekaa kwenye viti huku taratibu nyingine ndogo ndogo zikiendelea ili uchaguzi uanze saa nne kamili. Wanafunzi walikuwa wengi, kila aliyejaribu kutema mate, alimtemea jirani yake.

Ta! Ta! Ta! Ta! Ta ! Mshale wa saa kubwa ya kijani iliyokuwa imetundikwa kule mbele ulifanya kazi yake ipasavyo. Kila mtu alimchagua aliyemuona anafaa kulingana na sera zake. Ulifanyika uchaguzi wa wabunge pamoja na mawaziri ambao wangehudumu katika wizara mbalimbali. Uchaguzi ulimalizika kwa kupigwa kura za wale waliokuwa wakiwania nafasi ya juu kabisa pale Giazi, nafasi ya urais. Baada ya uchaguzi, Kaunda alipanda gari na kutokomea kusikojulikana. Hakuwa sawa hata kidogo.

Jioni, uvumi ulikuwa umesambaa kuhusiana na matokeo ya wabunge na mawaziri. Urais, haukusemwa kwa maneno yaliyofanana, kila mmoja alisema alichoona ni sahihi kwake. Wengi walidai Jamali ameshinda na wengi walidai Kaunda ameshinda. Wachache walidai Jamali ameshinda na wachache walidai Kaunda ameshinda.

Majira ya saa moja usiku, watu wote walikuwa ukumbini kupata kauli moja. Walikaa kimya kama wanafunzi wanaofanya mtihani. Upande wa kushoto, wakiwa ndani ya suti kali nyeusi, walikaa wagombea kusubiri mavuno ya kilimo chao asubuhi ile. Baadhi walifunikwa na nyuso za furaha kana kwamba tayari walijua matokeo. Baadhi walifunikwa na wingu zito katika nyuso zao, wingu lililowazuia kuona mbele.

Kaunda alikuwa katika hali isiyofasilika, huzuni au furaha. Alionekana kama kondoo aliyenyeshewa na mvua. Alihitaji kuinuka pale alipokuwa amekaa lakini alishindwa. Utumbo wake ulimchoma sana utafikiri alikuwa amekula pilipili. Alitetemeka sana huku moyo ukidunda kwa kasi kiasi cha kupasuka kama vile alikuwa amemuona simba.

‘Aaah, nakuona Kaunda, mbona una huzuni hivyo? Au umeshajua utashindwa tena kama mwaka jana? Haaa! Haaa! Haaa!’ Alisikia sauti aliyoitambua.

‘Tafadhali sana Nyabubu, naomba uniache kwa sababu siko sawa kabisa!’

‘Lazima usiwe sawa, unadhani utashinda? Kwa fikra na mawazo yako unadhani una uwezo wa kumshinda Jamali? Yule ni mjanja na ana mbinu nyingi lakini wewe sasa! Ha ! Ha ! Ha ! Kubaliana na mimi tu huwezi kushinda ! Ha ! Ha !’ Alicheka kwa dharau.

‘Nishinde, nishindwe, wewe inakuhusu nini? Mbona siyo mwelewa ? Nimekwambia uniache, mbona bado unanisumbua ?’

‘Mimi sikusumbui, ila nakwambia tu ukweli ! Unapoteza muda wako’

‘Unajua siku zote fanya juu chini uhakikishe watu hawajui kama huna akili.’

‘Kaunda, kwahiyo mimi sina akili si ndiyo ?’

‘Hayo umesema wewe!

‘Kwahiyo ulikuwa unamaanisha nini kusema hivyo? Yaani unaniambia sina akili! Subiri tu, nitakuonyesha.’ Aliondoka kwa hasira.

Nyabubu alipenda sana utani lakini alishindwa kutambua kitu kimoja tu kwa wale aliokuwa akiwatania, kusoma nyakati, alishindwa kujua kama mtu ana furaha au huzuni. Daima alileta utani tu, aligombana na watu wengi. Kila mara alipoambiwa akae mbali alifanya kinyume, wengi walichukizwa na tabia yake hii. Licha ya hayo yote, hakuwa mtu wa visasi kwa sababu alipenda sana utani. Angekorofishana na mtu asubuhi kwa sababu ya utani lakini mchana na jioni angemtania tena. Kaunda alimjua vizuri, ndiyo maana hata hakushituka alipomwambia atamuonyesha, kwa umri wake ni nini bado hajawahi kukiona katika maisha yake hadi Nyabubu amuonyeshe?

‘Hivi kweli nitashinda huu uchaguzi?!? Mhm! Sasa nitaificha wapi sura yangu? Kweli nitasoma tena kwa bidii? Sidhani kama nitashinda maana najua yale siyo maneno matupu ila ni ukweli, Jamali ameshaandaliwa tayari kuwa rais. Kweli mimi ni mtu wa ajabu, sasa kwanini niligombea na wakati naona kabisa siwezi kushinda ? Kila mara, nilikuwa namwambia Makame tuachane na haya mambo lakini akawa analazimisha tu, sasa leo si nitaaibika…’ Kabla hajamaliza mawazo yake, alishitushwa na sauti kubwa ukumbini mule.

‘Habari za jioni, naona nyote mna sura za furaha.’ Alitania kidogo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kisha akaendelea na mazungumzo yake. Alitangaza matokeo ya wabunge na mawaziri ambapo kila mara watu walishangilia kwa kelele na vifijo. Alitangaza matokeo yote hadi alipofikia kutangaza matokeo ya urais ambapo hali ya hewa yote ilibadilika ukumbini mule.

Kaunda alitamani kuinuka na kutoka ukumbini ili asijue matokeo yatakayotangazwa lakini alishindwa, angewezaje ? Alikuwa ni miongoni mwa wagombea, alitakiwa kuwepo wakati wa kutangazwa matokeo. Kiti alichokuwa amekalia kilimuwasha kama vile kilikuwa na miba, hakuweza kukikalia tena ! Lakini angefanyaje ? Alibaki tu ametulia huku akiwa amejiinamia chini.

‘Sasa ninamalizia hatua ya juu na ya mwisho kabisa.’ Kulikuwa na ukimya kidogo. ‘Katika mchuano huu, kulikuwa na wagombea wawili, Masenyi Kaunda na January Jamali ambapo walichuana vikali sana kiasi kwamba mshindi alimzidi mwenzake kura chache tu. Jumla ya kura zilizoharibika ni 1,407 na Masenyi Kaunda amepata jumla ya kura 18, 378.’

Matokeo yalipelekea ukumbi mzima kulipuka kwa furaha. Watu walipiga makofi hadi mikono ikakataa, haikutaka kupiga tena makofi. Kaunda hakuweza kuinua kichwa chake kwa sababu bado matokeo yaliendelea kutangazwa. Mwisho watu walinyamaza kabisa. Mwenyekiti alivuta pumzi kidogo watu wanyamaze kabisa ili aendelee. Baada ya kujiridhisha aliendelea ‘January Jamali amepata jumla ya kura 25, 4…’ Kabla hajamaliza kutaja namba zote, ukumbi mzima ulijaa shangwe na kelele.

Kaunda alianguka kabisa kutoka pale alipokuwa amejiinamia, alikosa nguvu. Baada ya muda, alijitahidi akainuka na kujikokota na hatimaye alifanikiwa kutoka ndani ya ukumbi ule. Baadhi ya marafiki zake walimsaidia kumshika mkono na kumpeleka chumbani kwake maana hakuwa na nguvu kabisa, alilewa bila kunywa chochote.

‘Haya niliyajua! Nilijua tu itakuwa hivi ndiyo maana sikutaka kuendelea na haya mambo. Sasa kama hii siyo aibu ni nini? Uchaguzi gani huu mtu anakuzidi kura elfu saba halafu bado kuna mtu anasema eti walitofautiana kwa kura chache tu!’ Aliigiza maneno yale kwa kutolea sauti puani kwa hasira.

‘Usiseme hivyo Kaunda, hii yote ni mipango ya Mungu.’ Alishitushwa na sauti ya Elisha aliyekuwa chumbani mule. Kaunda aligeuka na kubaki amepigwa na butwaa kwani aliamini kuwa alikuwa chumbani mule peke yake na yote aliyoyaongea hakujua kama aliyaongea kwa sauti. Aliona yalikuwa ni mawazo yake tu, hakujua kama aliwaza kwa sauti. Alishangaa kuona watu kama sita chumbani mule.

‘Hawa nao wamefikaje humu?’ Aliwaza tena kwa sauti.

‘Tumekuja na wewe, hukuwa vizuri kuanzia kule ukumbini kwahiyo tukaona tukusindikize hadi huku’ Alijibu Denis.

‘Eti sikuwa na nguvu kuanzia ukumbini ndiyo hadi nikasindikizwa?!?’ Safari hii aliwaza kimya. Ulipita muda kidogo kisha akasema ‘Nilijua tu sitashinda huu uchaguzi kwa sababu Jamali alikuwa ameandaliwa tayari! Nilidhani yalikuwa maneno ya watu tu ila saa hizi ndiyo naamini yalikuwa ni maneno ya kweli.’

‘Hapo sikubaliani na wewe kabisa! Mimi naamini siku zote kitu ambacho umekikosa basi siyo kizuri kwako na ilipangwa ukikose na unachokipata ni kizuri kwako na ilipangwa ukipate. Hii yote ni mipango ya Mungu, sioni kama kuna haja ya kuhuzunika sana, kikubwa tu soma kwa bidii ufaulu mitihani yako maana kama ni uchaguzi ndiyo tayari ishakuwa hivyo.’ Alihitimisha Elisha.

‘Kaunda! Kaunda! Kaunda! Kaunda! Kaunda! Una kipindi saa hizi na hapa bado kama dakika kumi na tano tu!’ Kwa mbali aliisikia sauti ya Elisha usingizi.

‘Saa kumi na dakika arobaini na mbili! Nimelala masaa matatu? Hii inawezekanaje? Au saa yangu ndiyo iko mbele?’

‘Kaunda, hayo maswali hayana nafasi tena, hakuna muda wa kutosha! Muda umeshaisha, jiandae twende darasani.’

 

Comments

Popular posts from this blog

J’AIME LE FRANÇAIS. LIVRE DE L’ÉLÈVE POUR LA PREMIÈRE ANNÉE. ENSEIGNEMENT SECONDAIRE

UCHAGUZI WA AJABU