UCHAGUZI WA AJABU

UCHAGUZI WA AJABU SEHEMU YA PILI

Jengo namba nne ndani ya kitivo cha Insia na Sayansi za Jamii, lilikuwa na kumbi kubwa tano kwa ajili ya mihadhara. Ndani ya ukumbi wa Amico wenye uwezo wa kubeba takribani watu mia tano, kulikuwa na watu wanne waliokuwa wamekaa kuizunguka meza ndogo ya duara iliyojaa vitabu na madaftari. Walikuwa kimya wakizungumza sauti zisizosikika.

January Jamali, mgombea urais wa serikali ya wanafunzi, alikuwa amekaa na kamati yake ndogo huku kichwani mwake akiwa na uhakika kwa asilimia zote elfu moja atakuwa rais wa Giazi. Ni Waziri wa Mikopo anayesubiri kwa hamu kubwa kuachia nafasi hiyo ili ashike nafasi yenye hadhi kubwa, nafasi inayotamaniwa na kila mmoja. Mkabala naye, alikuwa amekaa Amimu Hamisi, mwanafunzi wa shahada ya Kijerumani ambaye pia ni rafiki yake mkubwa tangu utotoni. Tangu alipozaliwa, Amimu Hamisi alizaliwa na lugha za kigeni. Alipenda sana lugha za kigeni na kila mara alipoongea alichanganya na lugha ya kigeni hata kama asipoeleweka kwa wale wanaomsikiliza. Watu wengi walimuona kama mpenda sifa ila alizoea kusema huwezi kupendwa na kila mtu kwa sababu wewe siyo pesa. Tangu wakiwa watoto, yeye na Jamali walikuwa ni marafiki wakubwa sana. Walipendana wakadumisha urafiki wao wakaufanya kama wa jicho na mkono. Jamali akilia basi Amimu atamfuta machozi na Amimu akiumia basi Jamali atalia. Kulia kwake, alikuwa amekaa Christopher Bundala, mkurugenzi wake wa kampeni, ambaye yuko tayari kutumia kila mbinu kwa ajili ya ushindi wa kiongozi wake. Kushoto kwake, alikuwa amekaa Nasra, binti mdogo mweupe mrembo mfupi na mwembamba, aliyesumbua sana mashingo ya wanaume kila mahali alipopita. Alikuwa rafiki mkubwa na mtu muhimu sana kwa Jamali. Tangu wakiwa watoto, wazazi wao hawakuisha kuitana wakwe. Baada ya siku chache, kilio chao kitapata majibu.

‘Ndugu zangu, naamini nanyi ni mashahidi na mnaona kabisa namna siku zinavyojitahidi kushinda mashindano yake. Siku zinakimbia kweli yaani kama vile zinakimbizwa. Tulianza kampeni juzi tu lakini hadi leo zimebaki siku kadhaa tu kuelekea uchaguzi.’ Alisema Jamali. Aliwatazama wenzake kana kwamba alitaka waseme kitu halafu aendelee lakini walikaa kimya. ‘Tunaweza kufanya tathmini kidogo kuhusiana na mipango yetu na hatua ambazo tumeshapiga hadi sasa ili tuone tulitoka wapi, tumefika wapi na tunaelekea wapi?’

Wote walikaa kimya kusubiri amalize kuongea, baada ya kupita ukimya mfupi ndipo mmoja kati ya watu wale akajiweka sawa pale alipokuwa amekaa, akakohoa kidogo kuweka sawa koo lake na kusema ‘Mheshimiwa Rais.’ Alinyamaza kidogo kusubiri aitike ndipo aendelee. ‘Nataka nikuhakikishie kuwa zimebaki asilimia tano tu kutimiza asilimia tisini na tano ya wapiga kura wote. Takwimu hii ninaitoa baada ya kufanya utafiti mdogo kuona ni namna gani wanafunzi wa kozi mbalimbali wanazungumza kuhusiana na wewe. Nimegundua kuwa tayari wengi wako upande wako. Kila kitu kitakuwa sawa! Usijali kabisa kwa hilo Mheshimiwa, niseme tu tayari umeshapita.’ Alisema Christopher.

Jamali alitabasamu kidogo. ‘Sawa, lakini umejaribu kujiridhisha hali ikoje kwa upande wa hawa wenzetu? Ni nini kinaendelea?’

‘Bila shaka unamfahamu vizuri Gayo na pia unaifahamu vizuri kazi yake, habahatishi kazi zake. Ni mjanja sana! Sungura akasome! Ni mara nyingi tu amekuwa akinijulisha kila kitu kinachoendelea upande wa pili, kiukweli tayari tumewashinda. Hivi mnajua kuwa Kaunda ni mvivu sana kwahiyo hawezi kushika nafasi hiyo kamwe! Ni vile tu anatimiza wajibu wa Katiba ya Serikali ya Chuo, vinginevyo atadhalilika sana.’ Alisema Christopher kwa kujiamini.

‘Je suis tout à fait d’accord avec toi, ni vile tu Katiba inataka kuwe na mgombea zaidi ya mmoja ndipo uchaguzi ufanyike ndiyo maana Kaunda naye akagombea lakini kiuhalisia hata yeye anajua kabisa hawezi kushinda, kwani kilichomfanya ashindwe mwaka jana ni nini? Bila shaka ndicho kitakachomfanya ashindwe na mwaka huu. Mwaka jana alikuwepo Kalinga lakini akashindwa, sasa mwaka huu ndiyo atamshinda January Jamali? Hakushiba kwenye sinia atashiba kwenye kijiko? Kwa mwili ule nani atamkubali awe rais? Tuwe na rais mwembamba vile ambaye hata akipulizwa na upepo anaanguka? Vipi siku moja akiwa jukwaani anahutubia ghafla ukaja upepo mkali si tutapata kazi nyingine ya kumuwahisha hospitalini? Anatimiza tu matakwa ya Katiba! Ha! Ha! Ha! Lakini bado hatashinda na hapo ndipo ataona badala ya kutekeleza matakwa ya Katiba, hakuwa na lingine la kufanya zaidi tu ya kuyatelekeza! Haaaa! Haaaa! Kuna mambo yanafurahisha sana!’ Alicheka kwa dharau Amimu Hamisi aliyekuwa kimya muda mrefu akisikiliza maelezo ya Christopher.

Christopher Bundala, alikuwa na mwili mnene uliobebwa na kichwa chake kidogo kilichokuwa katikati ya mabega mawili membamba. Watu wengi walimtania mwili wake haukuwa na ushirikiano huku wengine wakiogopa kufuru na kuishia kusema kazi ya Mungu haina makosa. Alikuwa mfupi mweusi na machachari sana! Maneno hayakumuisha kinywani mwake kama dalali wa vyumba. Siyo mabishano ya kielimu pekee, bali hata katika mabishano ya kisiasa, alijua kupangilia hoja zake na kuzitetea. Mara zote alipojiingiza katika mabishano aliibuka kidedea. Aliwahi kupewa kalamu nyekundu lakini akabisha kuwa ni nyeusi hadi akashinda. Kwa tabia hii, watu wengi hawakupenda kabisa kujiingiza kwenye ubishi dhidi yake, mara nyingi waliamua tu kunyamaza na kuonekana wajinga kwake. Kwa kutambua kuwa asiyefanya kazi na asile, aliamua kuwa mkurugenzi wa kampeni wa Jamali ambapo alitakiwa kutumia uwezo wake wote kuhakikisha Jamali anashinda ili ateuliwe kuwa Waziri Mkuu. Ili kufanikisha ahadi hii, alijiundia kundi dogo la watu watatu ambao wangemsaidia kupata kwa urahisi taarifa zote za upande wa pili. Baraka na Humphrey, walikuwa na jukumu la kujifanya wanafunzi wa kawaida na kuuliza maswali magumu kwa wagombea wa upande wa pili. Walitakiwa kuuliza maswali ambayo hayana uhusiano kabisa na uchaguzi. Wakati mwingine waliomba waahidiwe vitu vikubwa ambavyo wanajua kabisa serikali ya wanafunzi haiviwezi kwa sababu siyo serikali ya nchi.

Marc, mgombea ubunge alipokuwa akiendelea na kampeni zake, alieleza sera zake kwa muda mrefu. Kabla ya kuteremka jukwaani, alitoa nafasi kwa watu kadhaa waulize maswali.

‘Mheshimiwa, mara nyingi baadhi ya wanafunzi hupungukiwa alama kadhaa kwenye kozi zao na hushindwa kufanya mtihani wa mwisho. Wakienda kwa wahadhiri kuomba kuongezewa alama hutukanwa, kugombezwa na kufukuzwa. Wengine hupigwa kabisa, ukiwa kama mbunge utatusaidiaje kwa hili?’ Aliuliza Baraka.

Alipigwa na butwaa, alibaki akiwa mdomo wazi, hakujua ajibu nini. Alijitokeza mtu mwingine mkono ukiwa juu akisisitiza aulize swali lake vinginevyo atalisahau. Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumruhusu.

‘Ahsante sana kiongozi, swali langu ni dogo tu, ni kuhusiana na wahadhiri ambao hawatoi nukuu, badala yake wanatuambia tukajitafutie wenyewe. Wao wana elimu kubwa sana, wengine ni madaktari na wengine ni maprofesa lakini wameshindwa kutafuta nukuu hizo na kutupatia, sisi na elimu yetu ya shahada tu, tutazipata wapi? Naomba msaada tafadhali.’ Aliongea Humphrey kwa unyenyekevu.

Alitetemeka. Kijasho chembamba kilimtiririka. Yalikuwa maswali ya mtego na alilitambua hilo. Kwa taratibu za Chuo, yeyote ambaye atakuwa hajafikisha alama hatakiwi kufanya mtihani wa mwisho, sasa yeye atawasaidiaje? Awaombee kwa wahadhiri jambo linaloenda kinyume na sheria na taratibu za Chuo? Atakuwa kiongozi wa aina gani? Mwanafunzi wa chuo kikuu hawezi kujitafutia nukuu?!? Huu ni uzembe wa hali ya juu. Atawezaje kujibu huo ni uzembe? Alikosa nguvu kabisa, akaanguka jukwaani. Alichukuliwa na wasaidizi wake akapelekwa kupumzika. Wanafunzi wakaingiwa na huruma na wengine wakamuona mbabaishaji katika sera zake. Sasa kiongozi gani anaulizwa maswali nyeti kama hayo anazimia badala ya kujibu? Nilijua tu! Hakuna kiongozi pale! Baraka na Humphrey wakaangaliana na kutabasamu, wakapeana ishara ya dole gumba.

Pia, walitafuta wanachuo wenye changamoto za kifedha na kuwapa chochote kitu. Walimfanyia kampeni Jamali aingie madarakani aboreshe maisha yao pale chuoni. Siasa ni mchezo mchafu, walifanikiwa kupata wanachuo kadhaa waliowaamini wakanaswa na mtego wao.

Gayo, alikuwa na kazi kubwa ya kutoa taarifa kuhusiana na vikao vyote vilivyoendeshwa na wagombea wa upande wa pili. Hila na ujanja kama sungura, hakutambulika alikuwa upande gani. Alipangua mambo mengi yaliyopangwa na upande wa pili.

Asubuhi moja, walipoenda kufanya kampeni kwa wanafunzi wa kozi ya sheria walishangaa kuwakuta wameshughulishwa sana na kazi za wahadhiri wao. Tangu lini watu wakafanya kazi kwa pamoja? Chuo ni sekondari ? Majadiliano huwa ni usiku sasa mbona leo asubuhi? Au kuna mtu katikati yetu anatusaliti? Mfululizo wa maswali ulipita katika ubongo wa Masenyi Kaunda. Kikulacho ki nguoni mwako!

‘Bibie, umekuwa kimya sana, mdomo utatoa harufu, hebu tuambie kuhusu mkutano wako wa jana.’ Jamali alimgeukia Nasra na kumtania kidogo kwa sababu alikaa kimya kwa muda mrefu.

‘Kwa upande wangu, naona mambo siyo mabaya kabisa. Nimeshaonana na kikundi chetu cha wanawake na nimewashawishi kadri ya uwezo wangu. Nimewapa ahadi za kila aina na wao wameshindwa kupambanua mbivu na mbichi. Wameshindwa kugundua kuwa kuna mengine niliwaahidi ambayo hayatekelezeki. Kwa asilimia tisini tayari wako upande wetu. Pia, nimezungumza na baadhi ya wafanyakazi wa hapa wakiwemo walinzi na wafanya usafi na nimewapa mpango mzima wa nini wanatakiwa kufanya siku hiyo. Nimempa Likuda kazi ya kuwatengenezea vitambulisho bandia ambavyo watavitumia siku hiyo. Pia…’

‘Hao wafanyakazi wako wangapi jumla?’ Kabla ya kumaliza maelezo yake, Jamali aliuliza swali la udadisi.

‘Kwa idadi ya haraka, wako kama mia hamsini hivi. Nitapata uhakika nitakapopata vitambulisho vyao ila naamini watazidi mia moja. Pia, kama alivyosema Christopher, hata mimi nimeanza kupata habari nzuri. Kwa sasa wanafunzi wanazungumza mengi tu mazuri kuhusiana na wewe. Wengine wanasema kama ulifanya vizuri ulipokuwa Waziri wa Mikopo, hali itakuwaje utakapokuwa rais?’

Ulipita ukimya mfupi kama mochwari. Kila mtu alimsubiri mwenzake aanzishe mazungumzo. Hatimaye Jamali akavunja ukimya huo.

‘Sawa, lakini bado hatuna haja ya kubweteka tukaacha kuongeza nguvu kwenye kampeni kwa hizi siku zilizobaki. Wao pia wanahitaji nafasi hii, hata kama wanatimiza tu matakwa ya Katiba, bado hatuwezi kujipa uhakika kuwa tumeshinda. Tusiridhike kabisa! Tutaridhika wakati tutakapokuwa tumeshinda.’

‘Tumesoma sana, mimi nadhani kwa sasa tupumzike au nyinyi mnaonaje jamani?’ Aliuliza Amimu.

‘Yaani kwa haya yote tuliyosoma ni lazima tufaulu mitihani yetu.’ Alisema Christopher.

‘Kweli kabisa, tumesoma kwa muda mrefu, saa hizi tutawanyike ili kila mtu akaendelee na shughuli zake.’ Alisema Jamali wakatawanyika.

 


Comments

Popular posts from this blog

J’AIME LE FRANÇAIS. LIVRE DE L’ÉLÈVE POUR LA PREMIÈRE ANNÉE. ENSEIGNEMENT SECONDAIRE

UCHAGUZI WA AJABU